Job 6

Hotuba Ya Pili Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Malalamiko Yangu Ni Ya Haki

1Kisha Ayubu akajibu:
2 a“Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa,
nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!

3 bKwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote,
kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.

4 cMishale ya Mwenyezi iko ndani yangu,
roho yangu inakunywa sumu yake;
vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.

5 dJe, punda-mwitu hulia akiwa na majani,
au ng’ombe dume hulia akiwa na chakula?

6 eJe, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi,
au upo utamu katika ute mweupe wa yai?

7 fNinakataa kuvigusa;
vyakula vya aina hii hunichukiza.


8 “Laiti ningepata haja yangu,
kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,

9 gkwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda,
kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!

10 hNdipo bado ningekuwa na hii faraja,
furaha yangu katika maumivu makali:
kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.


11 i“Ninazo nguvu gani, hata niendelee kutumaini?
Matazamio yangu ya mbele ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?

12 jJe, mimi nina nguvu za jiwe?
Je, mwili wangu ni shaba?

13 kJe, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe,
wakati ambapo mafanikio yamefukuziwa mbali nami?


14 l“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,
hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.

15 mLakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,
ni kama vijito vya msimu,
ni kama vijito ambavyo hufurika

16 nwakati vimefunikwa barafu iyeyukayo,
ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,

17 olakini hukauka majira ya ukame,
na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.

18 Misafara hugeuka kutoka njia zake;
hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.

19 pMisafara ya Tema inatafuta maji,
wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri
hutazama kwa matarajio.

20 qWamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini;
wanafika huko, lakini wanahuzunika kwa kukosa walichotarajia.

21 rSasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wowote;
mnaona jambo la kutisha, nanyi mnaogopa.

22 sJe, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu,
au mnilipie fidia kutoka mali zenu,

23 tau niokoeni mikononi mwa adui,
au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’?


24 u“Nifundisheni, nami nitanyamaza kimya;
nionyesheni nilikokosea.

25 vTazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli!
Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?

26 wJe, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema,
na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo?

27 xMngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima,
na kubadilishana rafiki yenu na mali.


28 y“Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi.
Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?

29 zTulizeni hasira, msiwe wadhalimu;
angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu.
Au: haki yangu bado inasimama.


30 abJe, pana uovu wowote midomoni mwangu?
Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?

Copyright information for SwhKC